Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Kimetangaza kutoshiriki kwenye chaguzi ndogo za Madiwani katika kata 14 zilizotangazwa na tume ya taifa ya Uchaguzi
Taarifa iliyotolewa na chama hicho inasema hivi
“Leo tarehe 14 Juni, 2023 Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Madiwani katika kata 14 zilizopo kwenye Halmashauri 13 nchini
Aidha, Tume imetangaza kuwa Ratiba ya kampeni itaanza tarehe 01-12 Julai, 2023 bila kuelezea ni kwanini Muda wa kampeni umefanywa kuwa mdogo kiasi hicho.
Uchaguzi huo utaendelea kusimamiwa na Wasimamizi wa Uchaguzi ambao ni Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya kinyume na uamuzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Haki za watu katika uamuzi wake wa tarehe 13 Juni, 2023 baina ya Ndugu Chacha Wangwe dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kesi namba 011/2020 uliotolewa na Majaji 10 wa Mahakama hiyo kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri kuwa Wasimamizi wa Uchaguzi ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mkataba wa Afrika ambao Tanzania iliuridhia.
Wakati uamuzi huu wa Mahakama ya Afrika haujatekelezwa na Serikali, Tume imetangaza uchaguzi mdogo na kuwa utasimamiwa na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya.
CHADEMA tunatangaza kuwa hatutashiriki katika uchaguzi mdogo wa Madiwani uliotangazwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi.
Tunaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tume ya Taifa ya uchaguzi kuheshimu uamuzi wa Mahakama ya Afrika na kutekeleza uamuzi huo kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi wowote nchini
Vilevile, tunaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kuharakisha mchakato wa kuipata Katiba Mpya ambayo itakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na mabadiliko mengine ambayo yataweza kusimamia uchaguzi ulio huru na haki nchini.
Tunatoa wito Kwa watanzania wote kupaza sauti zao na kuunganisha nguvu za pamoja ili kuhakikisha kuwa Katiba Mpya inapatikana mapema iwezekanavyo.”
FOLLOW US HERE