Safari ya Mbappe katika nchi yake ya asili, Cameroon

 



Nyota wa soka wa Ufaransa, Kylian Mbappé, ameonyesha heshima yake kwa nchi yake ya asili Cameroon, kwa kuitembelea. 


Amesema kwamba watu wamemwonyesha mapenzi mengi.


Awali, mashabiki wa soka walielezea msisimko wao kuhusu safari hiyo katika mahojiano na kituo cha habari cha BBC. 


"Tumekuwa tukisubiri wakati huu na hatimaye umewadia," mtu mmoja alisema katika kipindi cha redio cha BBC Newsday.


"Ni msaada mkubwa kwa Cameroon, si tu kwa Cameroon bali kwa bara zima," shabiki huyo aliongeza. "Kuwa naye karibu kunathibitisha kuwa nyumbani ni nyumbani - lazima urejee nyumbani kwako."


Mbappé, nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa na mshambuliaji wa Paris Saint-Germain (PSG), ambaye alizaliwa Paris, Ufaransa, na baba Mcameroon, pia alikutana na Waziri Mkuu wa Cameroon, Joseph Ngute, siku ya Ijumaa, pamoja na maafisa wengine. 


Hii ni safari yake ya kwanza nchini Cameroon tangu akiwa kijana.


Nyota huyo wa soka alizungukwa na mamia ya mashabiki wenye shauku alipowasili Cameroon siku ya Alhamisi. Pia amekutana na wanamichezo wengine wa Cameroon, kama vile nyota wa MMA, Francis Ngannou, ambaye walipiga picha pamoja wakiwa wamefurahi.

Aidha, alishiriki mchezo wa mpira wa kikapu na nyota wa zamani wa Chicago Bulls, Joakim Noah, katika uwanja wa Noah, ambapo walipigwa picha na umati wa watu waliokuwa wakifuatilia mchezo huo.


Baadaye, alishiriki mchezo wa soka dhidi ya timu ya Cameroon, Vent d'Etoudi FC, kama ilivyoripotiwa na Reuters.


Mbappé pia anajihusisha na shughuli za kibinadamu katika safari yake kwa niaba ya taasisi yake, ambayo inalenga kuwasaidia vijana kufikia malengo yao.